Final Version Maswali 20 muhimu kuhusu bajeti ya kaunti yako

Shughuli ya bajeti ya mwaka 2014/2015 ilikumbwa na changamoto nyingi lakini kaunti zilifanikiwa kutoa mwongozo wa mipango ya fedha kwa mara ya kwanza na kaunti nyingi ziliandaa bajeti zao kwa kuzingatia mwongozo huu. Zaidi ya yote, kama inavyohitajika na sheria ya mwaka 2012 kuhusu matumizi ya fedha za umma, kaunti nyingi mwaka huu zilitengeneza bajeti kwa kuzingatia Program Based Budgeting (ratiba ya utekelezaji).

Huku kaunti zikikamilisha shughuli za kutengeneza bajeti zao, ni wakati mzuri wa kuanza kuzichunguza bajeti hizo. Ili kuwasaidia wananchi na mashirika katika kiwango cha kaunti kuelewa bajeti zao, tumeboresha mwongozo wetu wa “Maswali 16 Muhimu Kuhusu Bajeti” ili kuufanya uwe na maswali 20.

Hili lilichochewa pakubwa hasa na haja ya kutaka kutoa mwongozo zaidi kwa wale wanaosoma bajeti inayozingatia ratiba ya utekelezaji, ambayo ni tofauti sana na bajeti ya orodha ya matumizi ya kawaida kama vile mafuta ya gari, karatasi, kalamu na kadhalika. Japo kaunti zitakuwa zimefanya mabadiliko ili kutengeneza bajeti kwa kuzingatia mtindo wa kimpangilio, mwongo zo wa maswali 16 muhimu ungalipo (pamoja na mifano mingi ya namna mwongozo huu ulivyotumika).

 

Huku tukiwahimiza wananchi na wabunge wa kaunti kutumia mwongozo huu wa maswali 20 muhimu kutathmini bajeti zao, tunawahimiza pia kuendelea kufuatilia utekelezaji wa bajeti, kwani, mapendekezo ya bajeti na bajeti zilizoidhinishwa ni mwanzo tu wa shughuli nzima ya bajeti.